MAPENZI YA RAHA AU KARAHA, MWAMUZI NI WEWE!

BILA shaka utakuwa mzima wa afya njema, karibu katika safu yenu ambayo huboresha uhusiano na wenzi wetu. Mpenzi msomaji wangu, mapenzi yana raha na karaha zake. Huo ni ukweli ambao hauwezi kubadilishwa, lakini pamoja na hayo, raha ya mapenzi ni furaha. Huwezi kuwa kwenye mahusiano yenye matatizo kila siku. Hata hivyo, yanaweza kuwa karaha ikiwa  utaamua iwe hivyo. Ni suala la kuamua tu. Inawezekana kero zikasababishwa na sisi jinsi zote - wanaume au wanawake.
Lakini kitu cha msingi ni kutulia na kuangalia namna ya kujenga furaha ya kudumu kwenye mapenzi.
Katika mada hii nitakupa mbinu madhubuti ambazo zitakufanya ufurahie mapenzi siku zote.
BILA UAMINIFU, SAHAU!
Hapa nazungumzia uaminifu wako wewe kama wewe. Je, unao au unaishi kama ndege? Unajua mtu ambaye siyo mwaminifu huwa hapendi hata kuonekana hovyo, akipita hapa sasa hivi hutamwona hadi baada ya wiki mbili, yaani anakwepa watu!
Ukianza kukosa uaminifu wa kawaida hata amani ya moyo wako inakuwa vigumu kuwa nayo. Fikiria kama huna amani na huaminiwi utaweza kuwa na uaminifu katika mapenzi kweli?
Uaminifu wako kwa mpenzi wako, kuwa wazi kwake kwa kila kitu kunakuweka katika wakati mzuri wa kuyafurahia mapenzi. Mathalani mpenzi wako akishika tu simu yako inakuwa balaa!
Unadhani kutakuwa na furaha katika penzi la aina hiyo kweli? Ni vigumu sana. Hapo ndugu yangu utasubiri sana!
Uaminifu ni mwanzo mzuri wa kufurahia mapenzi badala ya kukukera, maana kama wewe siyo mwaminifu, ukisikia mpenzi wako anakutembelea bila taarifa tayari umeshakuwa mkali na hii ni kwa sababu ya ukicheche wako.
Unafikiri muda wowote unaweza kufumaniwa. Kwa staili hiyo mapenzi kwako yataendelea kuwa machungu siku zote za maisha yako.
LAZIMA UTAFUTE AMANI YA PENZI LAKO!
Sijui kama umeshawahi kusikia juu ya amani ya mapenzi, lakini kama hujawahi kusikia acha sasa nikuambie kuhusu amani ya mapenzi. Unaweza kuwa na amani na kila mtu, ukawa na amani mahali pako pa kazi, lakini ukakosa amani ya mapenzi.
Hili ni tatizo kubwa sana katika maisha ya binadamu maana maisha ya binadamu yametawaliwa kwa kiasi kikubwa na mapenzi, sijui naeleweka vizuri jamani?Usigombane na mpenzi wako kila wakati, usitafute ugomvi usio na maana, wakati wote ishi vizuri na mpenzi wako.
Kama amekukosea mwambie kuliko kumnunia maana kufanya hivyo hakutakusaidia lolote zaidi ya kuishi bila kuwa na amani ya mapenzi.
Jambo lingine la kuzingatia ni kwamba kama umeanzisha uhusiano na msichana na ukawa huna uhakika wa kuishi naye, usimhakikishie hilo. Kumpa uhakika ambao unajua moyoni mwako hauko, siyo sawa. Tafuta maneno mengine ya kuzungumza naye.
Mathalani unaweza kumwambia: “Kwa kweli mpenzi wangu nakupenda sana, siwezi kuishi bila wewe lakini suala la ndoa naomba tuliache kwanza, Mungu akipenda tutaoana lakini kwa sasa acha tuangalie maisha yetu kwanza.”
Kauli kama hii ni rahisi sana kuingilika akilini mwa mtu na akakuelewa.
Kwanza atajua wazi kuwa unamaanisha upo naye kwa ajili ya mapenzi ya muda tu, suala la ndoa ni majaaliwa! Siku zote ukweli huwaweka watu huru.

0 comments:

Post a Comment