NAJUA nitawakera wengi sana kwa kuandika habari
zinazomhusu Wema Sepetu, msichana mwenye jina kubwa Bongo, lisilofanana
na kazi anayoifanya, kwa sababu wapo wanaompenda sana na wengine
wamechoshwa naye.
Jumatatu wiki hii, Wema alifanya kituko cha mwaka, tena safari hii,
akizifuata kamera yeye mwenyewe, bila shaka baada ya kuona picha zake
nyingi tulizonazo hazitoshi. Akiwa na hasira, msichana huyo aliibuka
chumba chetu cha habari kama utani vile.
Walinzi walimruhusu kuingia katika lango kuu akiambatana na wapambe
wake wachache dhaifu kwa vile waliamini kuwa alishafanya mawasiliano na
mmoja wa waandishi wetu kama inavyotokea mara nyingi. Lakini ghafla
akiwa ndani, akageuka mbogo, akitukana matusi mazito ya nguoni huku
alioandamana nao wakifanya.
Waandishi wetu na walinzi walijaribu kumsihi atulize mzuka, lakini
hakusikia. Hata hivyo, waliendelea kuwa watulivu hadi askari Polisi
walipofika. Kwa kuamini kuwa ana matatizo ndani ya kichwa chake, uongozi
uliwashauri askari hao kuondoka bila kumchukua, kwani tayari hali
ilishadhibitiwa.
Tukio hilo limemalizika kimya kimya kwa sababu kampuni inaamini kwa
kumfungulia mashtaka, ya kufanya fujo ofisini na kutukana matuzi mazito,
itakuwa ni kumuongezea matatizo badala ya kumsaidia, kwani kwa kiasi
kikubwa, Wema anahitaji msaada wa kisaikolojia, ili akili yake ikae
katika mstari ulionyooka.
Huenda anaamini tayari yeye ni supastaa na sugu wa kesi, kwa vile
aliwahi kupata vikesi kama viwili vitatu na kushinda mahakamani. Kesi ya
kwanza ni ile ya kuvunja kioo cha gari la marehemu Steven Kanumba na
nyingine ni ya kumpiga meneja wa hoteli moja iliyopo Kawe jijini Dar es
Salaam ambaye alijaribu kumtuliza wakati akileta fujo eneo hilo, bila
shaka baada ya kulewa.
Siamini kama hizi ni kesi ‘siriaz’ ambazo mtu anaweza kujisifu kwa
kushinda, kiasi cha kumfanya kuwa kiburi wa kuamini anaweza kufanya
chochote mahali popote.
Wema Sepetu ni mmoja kati ya watu wenye bahati kubwa, ambao wanapaswa
kumshukuru Mungu badala ya kumkufuru, kwanza kwa kumpa umaarufu mkubwa
asiostahili na tena kwa kumnusuru na majanga mbalimbali kama hayo ya
kunusurika kwenda jela.
Katika hali ya kulewa au kupenda sifa kupitiliza, kuna wakati aliwahi
kutembea uchi jukwaani, hali iliyomfanya yeye na shoga yake, Aunt
Ezekiel kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kuomba radhi kwa
tukio lile.
Katika umri wake mdogo, ana msururu wa wanaume wanaofahamika
waliowahi kutoka naye kimapenzi. Nafikiri umefika wakati, mashabiki wake
kufanya sala maalum ya kumuombea. Huenda kuna vitu vinamsumbua kichwani
mwake kwa sababu baadhi ya matukio anayofanya, hayawezi kufanywa na mtu
mwenye akili ya kawaida tu.
Nimsihi kwa mara nyingine Wema, atulize akili yake. Kama anadhani
anaandikwa vibaya, hii yote ni kwa sababu yake mwenyewe. Watu
wanamfuatilia kwa sababu alipotwaa Umiss Tanzania mwaka 2006,
alijitengenezea sifa ya kuwa Public Figure. Na sifa hiyo akaamua
kuitumia vibaya. Mbona kuna mamiss kibao wamepita baada au kabla yake
lakini hawang’ai magazetini?
Asijiamini sana kwa sababu hana umaarufu wa kuishinda sheria na wala
hana mkwanja wa kumzuia mtu ‘mwenye nazo’ aliyepania kumtupa jela.
Katika nchi ambayo vyombo vyake vya dola na sheria vimeoza kwa rushwa
kama yetu, zoezi la kumpoteza kwa upuuzi anaoufanya wala halihitaji
ujuzi.
Ni vizuri akili yake ikakomaa kama mwili wake unavyokomaa, makosa ya
jana yampe somo ili aweze kuchukua tahadhari na kujifunza kwa sababu
maisha ya Uwema Sepetu yana mwisho.
0 comments:
Post a Comment