Kufanya jambo lolote la maudhi kwa mwenzi wako kwa makusudi ni jaribio la wewe kujuta baadaye. Unayemuudhi ni binadamu, ana moyo kama ulionao wewe. Siku atakapofanya uamuzi ambao anaona unafaa, itakuwa ndiyo mwanzo wa majuto yako. Kuwa mwangalifu sana unapopewa mapenzi yenye uzito.
NINI KILITOKEA BAADA GAUDENSIA KUACHANA NA REINA?
Dunia ina kawaida ya kurejesha majibu haraka, miezi sita baada ya Gaudensia kutimuliwa na Reina, tayari alikuwa ameshapata kazi nzuri katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), tayari alishajijenga sawasawa, akanunua kiwanja akiwa na ndoto za kujenga nyumba ndani ya miezi 10 inayofuata.
Reina alishafukuzwa kazi wakati huo, mambo yalishaharibika, wazazi wake hawakutaka kumuona. Mtaani alionekana kama kibaka kwa jinsi alivyochakaa. Maisha yalimdanganya, akarudi kwa Gaudensia kuomba msamaha. Kipindi hicho Gaudensia anaendesha gari lake aina ya Toyota Land Cruiser Parado milango mitatu.
Swali ni hili; Haya majuto ya Reina ya nini wakati alikuwa na nafasi ya kufanya uhusiano wake na Gaudensia uwe bora? Usimfanyie vitimbi mpenzi wako leo, maana hujui kesho yako ipo vipi. Majuto ya baadaye hayafai kabisa.
Niongeze hapo kwa kunukuu msemo wa Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela ambaye ni mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, aliye pia Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, John Samuel Malecela, aliyewahi kusema: “Ukimuacha mke unamuongezea PHD.”
Alimaanisha kuwa endapo utamfanyia vitimbi mwanamke wako kisha ukamtelekeza au kumwacha, usije ukadhani ndiyo utakuwa umemharibia maisha, badala yake ikae akili kwamba ukimfanyia hivyo unakuwa umemuongezea akili ya ziada. Usije ukashangaa baadaye ukikutana naye akiwa na maisha bora zaidi.
Hivyo ndivyo ilitokea kwa Gaudensia, akili yake ilifanya kazi zaidi baada ya kuachwa na Reina. Matokeo yakawa kinyume kabisa. Reina akawa anachunga muda wa Gaudensia kurudi nyumbani kwake kisha anakwenda kujibanza getini kuomba msamaha.
Kwa nini ujute baadaye? Tumia vizuri fursa iliyopo sasa. Ikiwa ipo wazi kuwa mpenzi wako anakuheshimu na anakupenda, linda heshima hiyo kwa kutomfanyia mambo ya ajabuajabu, kwani gharama yake ni kubwa sana pale mambo yanapogeuka kama ambavyo ilimgharimu Reina.
WASOME HAWA NA MATALI
Matali alikuwa mwenye upendo mkubwa sana na Hawa. Alijitahidi kumpa huduma zote muhimu. Hisia zake zilikuwa wazi mno. Hawa hakugundua hilo mapema, matokeo yake ule upendo wa Matali aliugeuza fimbo. Alimtenda sana kiasi ambacho kuna wakati Matali alipoteza kabisa furaha ya maisha.
Hawa kwa kiburi tu kwamba Matali anampenda sana, kwa hiyo hawezi kumwacha, alimfanyia vitimbi vingi. Kwa mfano; Matali alimpigia simu Hawa ambaye kwa kujisikia tu hakupokea. Alipomtumia SMS nazo hazikupata majibu. Hawa aliamua tu kumfanyia Matali vibweka.
Hakuishia hapo, Hawa akaanzisha uhusiano wa pembeni na wanaume wengine. Matali apoona mambo magumu, ikabidi aachie ngazi. Mwanzoni Hawa hakujutia, aliona sawa kwamba amepewa nafasi ya kutanua na aina ya wanaume anaowataka.
“Sitaki mwanaume mzembemzembe mimi, nataka mwanaume aliye ‘fiti’ kimazoezi, mwenye ‘six-pack’ ambaye tukiwa hata ufukweni, akikaa kifua wazi analipa,” yalikuwa ni maneno ya Hawa akisema mwanaume anayemtaka si aina ya Matali.
Hawa akawa anajiachia na wanaume wenye six-pack. Miaka miwili baadaye akashtuka kukuta Matali yupo mbali sana kiuchumi. Kampuni yake ilishapata mafanikio makubwa. Hawa aligundua hayo wakati ambao wanaume aliowataka walishampa maumuvi makali.
Baada ya kuhangaika na dunia kwa muda mrefu, mapenzi yakiwa sawa na msumari wa moto moyoni mwake, akili ilikaa sawa, akaona atafute kazi ambayo itampa kipato cha kusogeza maisha yake mbele. Hakuna mwanaume mwenye six-pack hata mmoja aliyemsaidia chochote katika maisha yake.
Dunia ilimwendea mrama, siku moja akasikia tangazo la nafasi za kazi redioni. Alichukua anwani, akaandika barua, alipoitwa kwenye usaili ndipo akagundua hiyo kampuni aliyokwenda kuomba kazi, mmiliki wake ni Matali, mwanaume ambaye alimpa mapenzi yote yeye akayapuuza.
“Ujinga wangu wa kudanganywa na dunia umenikosesha mengi, leo nakuja kuomba kazi niwe mtumishi wa kawaida, wakati kumbe ningemheshimu Matali na kuyatunza mapenzi yake, leo hii ningekuwa first lady wa hii kampuni yake,” aliwaza Hawa.
Baada ya kutoka kwenye chumba cha usaili, aliomba kumuona Matali. Katibu muhtasi alimjibu yupo ‘bize’ sana. Hata hivyo, wakati anageuka aondoke Matali alitoka ofisini kwake akiwa kwenye mwendo kasi, alipita anamuaga katibu muhtasi wake, akamwambia anakwenda kwenye mkutano ofisi ya uwekezaji, atarejea saa 9:30 alasiri.
Hawa pamoja na kumuona Matali yupo mbiombio, hakutaka kumpa nafasi, akamzuia mlangoni, akamwambia: “Please Matali, naomba unisikilize japo kwa dakika moja.”
Matali akamjibu: “Ooh Hawa, sikujua kama ni wewe. Ila kwa muda huu siwezi kabisa, njoo kesho saa 3:00 asubuhi tutatongea au ukiweza, urudi baadaye saa 11:00 jioni.” Baada ya kumjibu hivyo, Matali alimuunganisha Hawa na katibu muhtasi wake.
Hawa hakutaka kwenda nyumbani, alizungukazunguka, saa 10:30 alasiri alirejea ofisini kwa Matali. Saa 11:00 alikuwa kwenye kiti anatazamana na Matali. Alipigwa na mshangao kukutana na ofisi nadhifu ambayo ilionesha wazi kuwa inatunzwa kwa gharama kubwa.
Bila aibu, Hawa alishindwa kuvumilia akaanza kuomba msamaha. Alikumbuka mengi kutoka kwa Matali, akakiri kuwa ni mwanaume wa kipekee kwake, aliyekuwa na mapenzi ya kiwango cha juu mno kuwahi kutokea katika maisha yake. Alitamani yote ya nyuma yajirudie.
Ni kipindi ambacho aligundua kumbe Matali ni mwanaume mzuri, ana sura nzuri, umbile la kiume, mrefu. Mwanzoni kwa tamaa za dunia hakuyaona yote. Ni hapo ndipo swali linafuata; Kwa nini Hawa anajuta baadaye wakati alikuwa na fursa pana akaichezea?
HITIMISHO
Mapenzi ni fursa, jaribu kumheshimu na kumlinda uliyenaye. Wengi hutambua uzuri wa wapenzi muda mrefu baada ya kuharibu. Zingatia hisia za mwenzi wako, anapokwambia anakupenda, jaribu kuheshimu. Usithubutu kumtenda maana ukifanya hivyo ni lazima itajirudia kwako baadaye na kujuta.
Tambua kwamba mpenzi mbaya ni kwa sababu upo naye, akishaondoka halafu ukakutana na wabaya wenyewe, akili itakurejesha kwa yule uliyemchezea kisha utaanza kujuta ila majuto ni mjukuu! Bahati mbaya ni kwamba unaweza kutaka kurudi kwake kipindi ambacho ameshawahiwa na anayemthamini kwelikweli.
0 comments:
Post a Comment