MKE ACHOMA NYUMBA KISA WIVU WA MAPENZI:




KATIKA hali ya kusikitisha, mwanamke mmoja mwenye ujauzito wa miezi 7 sasa, Vaileth Kibwana, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mjini hapa baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kuiteketeza nyumba yao kwa moto, katika kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi baina yake na mumewe.
Mume wa mwanamke Vaileth Kibwana, anyeshikiliwa na jeshi la polisi kwa kuchoma moto nyumba yao  na kuteketeza mali nyingi kwa kisa cha wivu, akiwa katika hali ya taharuki kutokana na madhara yaliyotokea. 
Tukio hilo lililotokea Aprili 5, mwaka huu, majira ya saa 7 mchana katika mtaa wa Mji Mwema eneo la Nanenane, limesababisha uharibifu mkubwa wa mali, zikiwemo fedha ambazo idadi yake haikuweza kujulikana mara moja, pamoja na mali za wanafunzi watano wa Chuo Kikuu cha Jordan kilichopo mjini hapa, ambao walikuwa wamepanga ndani ya nyumba hiyo.
Raia wakishuhudia magari ya kikosi cha zimamoto yakiwasili eneo la tukio ili kutuliza moto ulioteketeza nyumba.
Mmoja wa wanafunzi hao, Richard Talimo alisema siku ya tukio alimuona mama mwenye nyumba wake akiwa na dumu lenye mafuta ya petrol, lakini hakuweza kumtilia shaka kwa vile anafahamu kwamba familia hiyo inamiliki magari na pikipiki.
Mmoja wa zimamoto akizima moto ambao tayari ulikuwa umekwisha teketeza sehemu kubwa ya nyumba hiyo.
“Nilimuona akichoma godoro na baadaye nyumba nzima, mimi na mwenzangu Jafari Yahya tuliacha vitu vyote na kuchukua CV zetu na kukimbia nje, wenzetu watatu Abdul Busagala, Issac Petro na Abel Abel ambao walikuwa shule vitu vyao vyote viliteketea.
Moja ya chumba cha nyumba iliyoteketezwa kwa moto.
“Kinachoniuma ni kwamba juzi wazazi wangu walinitumia ada laki sita ambazo nilipanga kesho yake nikalipe chuoni,  nimeamua kuzisamehe ziungue, nikaamua kuchukua CV zangu tu kwa vile ndizo muhimu katika maisha yangu. Huyu mama ugomvi wake na mumewe unatuhusu nini sisi? Angetuambia tutoe vitu vyetu ndipo achome nyumba yao,” alisema Richard.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Said Korongo alilizungumzia tukio hilo na kusema wanandoa hao wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara kwa kipindi kirefu, kwani kwa mara ya mwisho Alhamisi iliyopita, alipata kesi ya mwanamke huyo kuchoma moto pikipiki na nguo za mumewe katika ugomvi wa wivu wa mapenzi.
Mjumbe wa serikali ya mtaa, Amina Magoma.
“Nilimwambia mwanaume aende akaripoti polisi, akaenda usiku huo huo, kesho yake akaja na barua ya wito wa polisi, nikampa, leo tena nashangaa amechoma moto nyumba,” alisema Korongo na kuongeza kuwa wanafunzi hao watano wamehifadhiwa nyumbani kwa mjumbe wa serikali ya mtaa huo, Amina Magoma.
Habari zaidi zilizopatikana eneo la tukio zinasema pamoja na vitu vingine, ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na fedha za mkopo ambazo mume wa Vaileth, Regan Leonard alikuwa amekopa katika benki moja mjini hapa na kwamba mwanamke huyo alijua uwepo wa fedha hizo zinazodaiwa zililenga kununua basi dogo la kusafirishia abiria aina ya Coaster.
Mwenyekiti huyo wa mtaa alishindwa kuthibitisha habari hizo, lakini mwandishi wa habari hizi aliwashuhudia watoto wakigombania vipande vya noti za shilingi elfu kumi vikiwa vimezagaa ndani ya mojawapo ya vyumba vya nyumba hiyo baada ya moto huo kuzimwa na Zimamoto.
Regan Leonard alipoulizwa juu ya jambo hilo alishindwa kulizungumzia kwa madai kuwa mkewe alifanya ukatili mkubwa unaohitaji muda wa kutafakari kabla ya kuongea kwani ni kama amechanganyikiwa.
Wanandoa hao ni wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro na walifunga ndoa yao katika Kanisa Katoliki mkoani hapa na wamejaaliwa kupata mtoto mmoja aitwaye Feidhi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwa sasa wanamshikilia mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 25 na kwamba baada ya kukamilisha uchunguzi wao, watampandisha kizimbani.

0 comments:

Post a Comment