JOHARI,OSTAZ JUMA VITANI:

NI mtafutano! Staa mkubwa wa sinema za Bongo, Blandina Chagula ‘Johari’ ameingia kwenye vita ya maneno na bosi wa Mtanashati Entertainment, Ostaz Juma Namusoma ikiwa ni siku chache tangu jamaa huyo alipotangaza kumuoa mwanadada huyo.
Staa mkubwa wa sinema za Bongo, Blandina Chagula ‘Johari’.
Wakizungumza na Risasi Jumamosi kwa nyakati tofauti, kila mmoja alitoa la moyoni huku Johari akionekana kukasirishwa mno na ishu hiyo.
KILICHOMPONZA JOHARI
Ilidaiwa kuwa baada ya Ostaz kutangaza kwamba atafunga ndoa na Johari, vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii vililichukulia jambo hilo kwa ukubwa wake kwani mwanadada huyo hakufunguka sawasawa.
WENGINE WADAI KULIPA KISASI
Habari zinasema baada ya ishu hiyo kugeuka habari ya mjini ilidaiwa kwamba labda Johari aliamua kufanya hivyo kwa kuwa mkurugenzi mwenzake wa RJ Film Production ‘RJ’, Vincent Kigosi ‘Ray The Greatest’ naye alidaiwa ‘kuchepuka’ na Chuchu Hans.
Bosi wa Mtanashati Entertainment, Ostaz Juma.
Kuenea kwa habari za Johari kuolewa na Ostaz kulimsababishia usumbufu mkubwa mwanadada huyo kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki wakihoji ukweli wa ishu hiyo ili kujiandaa na cherekochereko.
MADAI YA AWALI YA OSTAZ
Katika maelezo yake ambayo yapo kwenye rekodi zetu, Ostaz alidai kuwa Johari anajua kila kitu kwani walifahamiana kitambo hata kabla ya mrembo huyo kujuana na Ray.
Hakuishia hapo, Ostaz alidai kuwa tayari amemfungulia Johari kampuni ya kutengeneza sinema pamoja na vifaa vyote hivyo yupo kwenye mishemishe za kumuoa.
JOHARI SASA
Ili kuondoa utata huo, gazeti hili lilimtafuta Johari kwa udi na uvumba na kutaka kujua undani wa ishu hiyo ambayo imezua maswali mengi hasa kwa mashabiki wake.Johari: Sijawahi, sina na wala siwezi kuwa na uhusiano na mtu mpuuzi kama yule (Ostaz Juma). Mwanzoni nilidhani utani, nashangaa imekuwa ishu kubwa.
Risasi Jumamosi: Kwani hufahamiani na Ostaz? Mbona anasema anakujua tangu unaishi Mburahati, Dar na enzi ukiwa Kaole?
Johari: Ni kweli Ostaz alikuwaga anakuja pale Kaole tulipokuwa tunafanya mazoezi lakini si yeye waliokuwa wanakuja ni wengi.
Risasi Jumamosi: Je, hajawahi kuleta maombi ya kukuoa?
Johari: Hakuwahi kunitongoza ila kila nilipokutana naye nilikuwa najua kwa kumwangalia tu machoni. Alikuwa anaonesha kabisa ananitaka lakini hakuwahi kunitamkia.
“Hajawahi kuniambia anataka kunioa. Kwanza mimi ni Mkristo. Sina ndoa mbili. Siwezi kuolewa mke wa pili na mpuuzi kama yeye.
Risasi Jumamosi: Je, zile picha zilizosambaa ukiwa umepozi kimahaba na Ostaz zilitoka wapi?
Risasi Jumamosi: Ilikuwa nje ya RJ, nilipiga picha na watu wengi kama Dogo Janja akiwemo na huyo Ostaz. Nilipigwa na butwaa nilipoziona mitandaoni eti nina uhusiano na Ostaz huku naye akiulizwa na kudai ni kweli.
“Kwani kupiga picha na mtu ndiyo tayari mmekuwa wapenzi au wachumba? Labda yeye anachukulia hivyo kwamba ukishapiga picha na mwanamke tayari anakuwa mpenzi wako.”
Risasi Jumamosi: Kuhusu dini, Ostaz alisema atakubali uwe Mwislamu na jina lako litakuwa Rahma. Je, alishakuambia juu ya hilo?
Johari: Hajaniambia, hata  hivyo, sina mpango wa kubadili dini ili niolewe na yeye.
Risasi Jumamosi: Vipi kuhusu Ostaz kukufungulia kampuni na vifaa vya kutengenezea sinema?
Johari: Mh! Achana na kampuni au vifaa, hata simu tu hajawahi kuninunulia, kwanza hana fedha. Halafu ajue kabisa kwamba mimi ni tofauti na hao wasanii wengine wanaoishi kwa kutegemea kuhongwa. Mimi ni super woman, siku hizi huwa fedha kwangu ni makaratasi. Huyo Ostaz ana fedha gani?
“Haniwezi, mimi siyo kama hao watoto anaowadhalilisha kwa kuwapigisha magoti na akome kabisa kutumia jina langu kama daraja. Hakuna kitu ninachochukia kama mtu kutaka kutumia jina langu kujitafutia umaarufu, ana hadhi gani ya kuwa na mimi, akome kabisa, mimi nimesota, ninyi Global mnajua.”
Risasi Jumamosi: Umekana kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Ostaz, je, una mchumba au mpenzi?
Johari: Mimi ni mwanamke niliyekamilika. Nina mchumba na ‘soon’ nitamtambulisha kwa mashabiki wangu. Lakini ijulikane kuwa siyo Ostaz kwani hawezi kuwa mchumba wangu.
Risasi Jumamosi: Au unataka kurudi kwa Ray?
Johari: (mshtuko) hivi ni nani aliwahi kutamka kwamba mimi na Ray ni wapenzi. Hapana, siyo Ray.
Risasi Jumamosi: Kwani Ray ni nani kwako?
Johari: Ray ni mkurugenzi mwenzangu wa RJ. Nje ya kazi tuna maisha yetu mengine.
Risasi Jumamosi: Je, ni mtu maarufu?
Johari: Nimeshasema nitawatambulisha subirini. Unajua mimi siyo mtu wa matangazo. 
Baada ya kumsikia Johari, gazeti hili lilimgeukia Ostaz ambaye hakupatikana, lakini rafiki yake wa karibu alidai kuwa Johari amechanganyikiwa kwani Ostaz alikuwa amuoe kweli lakini hamuelewi mwenendo wake wa sasa.

0 comments:

Post a Comment