YANGA YAMALIZANA NA MRITHI WA MBUYU TWITE:


Beki wa Yanga, Mbuyu Twite.

DALILI za wazi za Yanga kuonyesha kukata tamaa ya kuendelea kuwa na beki wake, Mnyarwanda Mbuyu Twite, zimefikia kwenye kiwango cha juu baada ya kukubali kuachia aondoke kwa kuwa imeshindwa dau analohitaji, lakini sasa imeenda mbele zaidi kwa kutafuta mrithi wake mapema.
Twite amekuwa akiwaniwa na Azam FC kwa muda mrefu na tayari ameshafanya mazungumo na viongozi wa klabu zote, lakini Yanga ndiyo wanaoonekana kukata tamaa na sasa Hamis Ramadhan Kessi wa Mtibwa Sugar anatajwa kuwa mrithi wake na tayari hilo limepitishwa.
Mtoa taarifa kutoka ndani ya Yanga ameliambia Championi Jumamosi kuwa uongozi wa Yanga umeamua kuweka nia ya kumsajili Kessi kwa kuwa haujaridhishwa na utendaji kazi wa beki mwingine wa kulia wa timu hiyo, Juma Abdul.
“Huyu Twite bado haeleweki muda wowote mambo yanaweza yakawa tofauti, kwa kuliona hilo Yanga wameamua kujipanga mapema na tayari wameshakubaliana kuwa Kessi atakuja kuchukua mikoba yake.
“Wameamua kufanya hivyo wakitumia kigezo cha kutoridhishwa na uwezo wa Juma Abdul ambaye naye pia hatma yake ya kubaki Yanga inasubiri hatma ya Twite kwanza.
“Kama Twite ataondoka Yanga basi Juma atabaki ili asaidiane na Kessi lakini kama atabaki basi safari itakuwa imemkuta kwa sababu tayari Yanga wamedhamiria Kessi aje kutokana na uwezo aliounyesha msimu uliopita, kwa hiyo hawawezi kukaa na mabeki wote hao,” kilisema chanzo hicho.
Alipoulizwa Kessi kuhusiana na hilo alijibu kwa kifupi akisema: “Siwezi kuzungumza chochote kuhusiana na hilo, nafikiri ni mapema mno kwa sasa.”

0 comments:

Post a Comment